UWANJA WA MAO TAYARI USHAANZA KUWEKWA NYASI BANDIA, SASA NI FURSA NYENGINE KWA WAZANZIBAR
Harakati
za Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni Mjini
Zanzibar zinaendelea chini ya Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai
Group ya Jamhuri ya Watu wa China na sasa wanaendelea na zoezi la uwekaji wa
nyasi bandia katika uwanja wa Soka.
Mtandao huu imeshuhuidia maendeleo ya uwanja huo yanavyoendelea ambapo kwasasa mafundi hao
wanatandaza nyasi bandia huku zoezi hilo likitarajiwa kukamilika muda mchache.
Tayari uwanja huo umeshawekwa Taa ambazo zitasaidia kuchezwa michezo hadi usiku huku baadhi ya vifaa vyengine vinazidi kutoa sura
mpya ya kukamilika kwa ujenzi huo kadri ya siku zinavyokwenda.
Ujenzi wa uwanja huo unafuatia msaada
mkubwa ulioidhinishwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika azma ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa pande hizo
mbili ukizingatia heshima uliopewa Uwanja huo wa kuitwa jina la Muasisi wa
Taifa la China Hayati Mao Tse Tung.
Uwanja huo utakuwa na Viwanja viwili vya mpira wa
miguu na chengine cha Mpira wa Kikapu, Mpira wa Mikono, Mpira wa Pete na na
michezo mengine ya ndani kama vile Mpira wa Meza pamoja na sehemu ya kufanyia
mazoezi ya kuinua vitu vizito.
Katika Viwanja hivyo vya Mpira wa Miguu uwanja mmoja
utakuwepo upande wa Magharibi ambao utakuwa na Jukwaa moja litakalochukuwa
Mashabiki 1500 waliokaa.
Uwanja mwengine wa mpira wa miguu utakuwepo upande
wa Mashariki ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua Mashabiki waliokaa 900 katika
jukwaa moja ambalo litakuwepo katika Uwanja huo.
Uwanja huo utagharimu Shilingi Bilioni 12.5 kwa
fedha za Tanzania ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itatoa Shilingi
Bilioni 11.5 huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia zaidi ya
Shilingi Bilioni 1 kati ya hizo Bilioni 12.5 ambazo watalipwa Wakandarasi wa
uwanja huo ambao ni Kampuni ya Zhengtar Group Company Limited ambayo ina uzoefu
mkubwa wa kujenga Viwanja wa Michezo.
Comments
Post a Comment