KOCHA WA KARUME BOYS ATAMBA KUBEBA UBINGWA WA CECAFA KUTOKANA NA KIKOSI CHAKE KILICHOSHEHENI VIPAJI
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka chini ya
miaka 17 (Karume Boys) Mzee
Ali Abdallah amewatoa
hofu Wazanzibar juu ya kikosi chao kinachotarajiwa kwenda Burundi katika
Mashindano ya CECAFA ya vijana yanayotarajiwa kuanza rasmi April 14 mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kumaliza mazoezi mchana wa leo
katika uwanja wa Amaan Kocha Mzee amesema wameamua kufanya mazoezi mchana ili
kuzowea mazingira ya Burundi katika Mashindano hayo kwani katika ratiba
wamepangiwa kucheza michezo mengine mchana huku akiwatoa hofu wa Wazanzibar na
kusema kuwa anaamini kikosi chake kitatwaa Ubingwa wa Mashindano hayo.
“Tunashukuru Mungu mazoezi yanaendelea vizuri mana Vijana
wanapokea vizuri mazoezi, tumeamua kufanya mazoezi mchana kwasababu kule
Burundi ratiba ya michezo yetu siku nyengine tunacheza mchana ili tuzowee
mazingira, mimi naamini vijana hawa kwa vile wanaari kubwa watabeba ubingwa na
Wazanzibar wasiwe na wasi wasi wowote”.
Aidha kocha Mzee amesema hana wasi wasi kwa timu zilizomo
katika kundi lao B huku akisema wao wanaamini watashinda bila ya woga wowote.
“Baadhi ya watu wanasema kundi letu B ni kundi la Kifo lakini
mimi sina wasi wasi wowote wa timu zile, sisi tunajivunia vipaji na vijana
wanahamasa ya kufanya vyema kama kaka zao Zanzibar Heroes”. Alisema Kocha Mzee.
Wakati huo huo kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar
Heroes) na Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Hemed Suleiman
(Morocco) amesema Zanzibar ina vipaji vingi hivyo anaamini kikosi cha Karume
Boys kitafika mbali katika Mashindano hayo.
“Mimi sina wasi wasi na vijana hawa kwasababu tuna program
nzuri ya Vijana na pia tuna vipaji, japo tumecherewa kuanza mazoezi na vijana
hawa lakini watafika mbali”. Alisema Kocha Morocco.
Mashindano hayo yanayotarajiwa
kuanza kutimua vumbi nchini Burundi April 14 hadi 28, 2018 ambapo Zanzibar imepangwa
kundi ‘B’ pamoja na ndugu zao Tanzania bara, Sudan na Uganda huku kampeni zake Zanzibar
kuwania kombe hilo zitaanza kwa kucheza na Sudan April 15 katika uwanja wa
Gitega majira ya saa 7:30 za mchana.
Comments
Post a Comment