DOKTA SHEIN AENDELEA KUPONGEZWA NA WADAU WA SOKA


Wapenzi wa Soka nchini Tanzania wanaendelea kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Wa Baraza La Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuwapa zawadi ya viwanja vya kujenga nyumba pamoja na fedha taslim Shilingi milioni tatu kwa kila mchezaji na kiongozi wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes).

Kupitia mitandao mbali mbali ya kijamii ikiwemo Twiter, Facebook, Whatsup mashabiki hao wa soka wamezidi kumimina pongezi wa Rais huyo kwa kuwapatia vitu ambavyo hawatovisahau Mashujaa hao walioshinda nafasi ya pili  kwenye mashindano ya Cecafa Senior Challenge yaliyofanyika nchini Kenya mwezi huu wa Disemba.

Jambo hilo limezuwa mijadala mingi mitaani huku kila mmoja akisifu uzalendo huo ulofanywa na Dk Shein ambapo Wanamichezo hao wengine walitokwa na machozi kwa furaha kubwa waliyopatiwa na Rais wao kwani hawakuamini zawadi nzuri na bora waliyopatiwa.

Dk Shein alizitowa zawadi hizo katika tafrija maalum iliyofanyika juzi Jumamosi katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni mjini Zanzibar sambamba na taarab maalum aliyowaandalia timu hiyo iliyotumbuizwa  na kikundi cha Taifa cha Taarab cha Zanzibar .

Dk. Shein alitoa zawadi hiyo kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa Ijumaa huko katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambapo akitoa salamu zake na pongezi kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo alikataa kuzitaja zawadi hizo na ambazo jumla yake zilikuwa tatu na aliitaja ile ya taaraab tu na kusema mbili angezitaja hapo juzi.

Kila mmoja ukumbini hapo alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa Dk Shein kuzitangaza zawadi hizo ambapo punde tu baada ya kutangazwa Vigeregere, hoihoi na nderemo zilisikika kutoka kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo pamoja na hadhara iliyohudhuria tafrija hiyo.

Dk. Shein aliwakabidhi hundi ya Shilingi za Kitanzania milioni tatu kwa kila mchezaji na viongozi ambao kwa ujumla wao ni 33 huku akiwaeleza kuwa kwa upande wa viwanja watakabidhiwa si muda mrefu baada ya kukamilika hati zao na nyaraka nyengine muhimu kutoka kwa Wizara husika ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.

Comments

Popular posts from this blog

HUYU NDIYE MCHEZAJI MWENYE REKODI YA KUFUNGA MAGOLI MENGI KWENYE MECHI YA TAIFA DHIDI YA BOYS

WACHEZAJI WA 5 WA ZANZIBAR HEROES WAMEITWA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA TAIFA STARS KWAAJILI YA MICHEZO MIWILI YA KIMATAIFA YA KALENDA YA FIFA.

KMKM KUANDAA MASHINDANO YA RIADHA