YAJUWE MATUKIO 10 MAKUBWA YA MICHEZO ZANZIBAR YALIOTOKEA 2017, YALOANDALIWA NA MWANA MICHEZO ABUBAKAR KHATIB KISANDU
1.YANGA KUCHAPWA 4-0 NA AZAM, AZAM
KUTWAA MAPINDUZI CUP MBELE YA SIMBA
(a) January 7,2017 katika uwanja wa Amaan Zanzibar, Yanga walipata kipigo ambacho
hawatokisahau mbele ya Azam Fc kwenye mashindano ya kombe la Mapinduzi baada ya
kuchapwa 4-0 na kupelekea kuwa kipigo cha pili kikubwa kwa Yanga kufungwa toka May 6 2012 alipofungwa goli 5-0
na Simba katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Magoli ya Azam FC siku
hiyo yalifungwa na nahodha wao wakati
huo John Bocco , Yahaya Mohamed Joseph Mahundi na Enock Atta.
(b) January 13, 2017 timu ya Soka ya Azam Fc ilitwaa Ubingwa
wa Kombe la Mapinduzi 2017 baada ya kuifunga Simba bao 1-0 kwa bao lililofungwa
na kiungo mkabaji Himid Mao Mkami dakika ya 13 mchezo uliopigwa katika uwanja
wa Amaan.
2.ZIMAMOTO NA KVZ KUCHEZA CAF NA KUTOLEWA
HATUA YA AWALI
Februari 19, 2017 wawakilishi wa Zanzibar na kwenye
kombe la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika timu ya Zimamoto na KVZ
zilitolewa katika hatua ya awali kwenye Mashindano hayo .
Kwenye klabu bingwa Zimamoto ilitolewa na timu ya
Ferroviario Beira ya Msumbiji baada ya kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wa
mwisho wa ugenini ambapo awali nyumbani walishinda 2-1 hivyo wakatolewa kwa
kufungwa jumla ya mabao 4-3.
Na kombe la Shirikisho timu ya
KVZ nayo ilitolewa katika mashindano hayo baada ya kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi
ya Messager Ngozi ya Burundi baada ya mchezo wa mwanzo uliochezwa Zanzibar KVZ
walishinda 2-1, hivyo walitolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 4-2.
3.ZANZIBAR KUPATA UANACHAMA
KAMILI WA CAF
Machi 16, 2017 ilikuwa ni siku ya furaha kwa Wazanzibar
ambapo katika mkutano uliofanyika Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia Shirikisho
la Soka Barani Afrika (CAF) lilitangaza kuwa Zanzibar mwanachama mpya kamili wa
55 wa CAF.
4.MJINI ZANZIBAR WATWAA TENA UBINGWA WA
ROLLING STONE
Julai 18, 2017 timu ya Kombain ya Mjini Unguja
imefanikiwa kutwaa tena kombe la Mashindano ya Vijana ya Afrika Mashariki na
Kati ya Rolling Stone baada ya kuichapa timu ya Fire Boys ya Karatu mabao 2-0
kwenye fainali iliopigwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo Mbulu Mkoani
Manyara.
5.ZANZIBAR YAPOKONYWA UANACHAMA WA CAF
July 21, 2017 ni siku ya huzuni kwa Wazanzibar baada ya
Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuwapokonya Zanzibar
uanachama wa kudumu wa 55 wa CAF, ambapo Rais wa Shirikisho hilo Ahmad Ahmad
alisema haiwezekani nchi moja (Tanzania) kuwa na wanachama wawili kwenye
shirikisho hilo, hivyo uanachama huo umedumu kwa siku 128 tu tangu Machi 16
hadi July 21, 2017.
6.MASHINDANO YA RIADHA YA KMKM YALINOGA
Oktoba 29, 2017 Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo
Zanzibar (KMKM) kilifanya Mashindano ya mbio za Kilimita 10 ambazo zilianzia Makao
Makuu ya KMKM Kibweni na kumalizika katika viwanja vya Maisara huku washiriki
kutoka Kenya, Tanzania bara na Zanzibar walishiriki.
7.KWA MARA YA KWANZA ZANZIBAR KUFANYIKA
SPECIAL OLYMPIC
Disemba 8, 2017 kwa mara ya kwanza Zanzibar yalifanyika
Mashindano ya Olimpik Maalum katika uwanja wa Amaan, mashindano hayo yanashirikisha
watu wenye ulemavu wa akili Tanzania nzima walishindana kwenye michezo mbali
mbali ikiwemo Soka na Riadha.
8.ZANZIBAR HEROES, KUSHINDA NAFASI YA PILI,
KUPOKELEWA KISHUJAA, KUPATIWA MILIONI 3 NA KIWANJA NA DK SHEIN
(a) Disemba 17, 2017 kwenye uwanja wa Kenyatta huko Machakos nchini Kenya
timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ilishinda nafasi ya pili kwenye
Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup baada ya kufungwa na wenyeji Kenya kwa
Penalty 3-2 kufuatia dakika 120 kwenda sare ya 2-2.
(b) Disemba 18, 2017 Zanzibar Heroes iliwasili nchini wakitokea Kenya katika
Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup ambapo msafara wa watu 45 ukiongozwa na
Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma uliwasili mchana
katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kwa ndege maalum ya
Kukodi.
Shangwe,
Chereko, vifijo na nderemo vilitawala maeneo yote ya mjini wa Unguja maelfu ya
wananchi na viongozi wa kiserikali walijitokeza kuwapokea mashujaa hao, licha
ya ndege iliyowabeba watu hao kuchelewa kufika kwenye uwanja wa ndege wa
Zanzibar (Abeid Amani Karume International Airport), kwa zaidi ya saa tatu
lakini umati wa watu haukupungua hadi timu hiyo ilipowasili majira ya saa sita
mchana, Kikosi hicho chini ya Kocha Hemed Suleiman Morocco, kilipowasili
kilipokelewa na kupakiwa katika magari ya kifahari huku misururu ya watu wengi
wakiwasindikiza kwa kuhinikiza shangwe na vigerere mpaka Mnara wa Kumbukumbu wa
Mapinduzi Kisonge Michenzani Mjini Unguja.
Tukio hilo lilionekana kuwa kubwa sana huku wananchi
wakisahaua kabisa tofauti zao za kisiasa na kuwa kitu kimoja katika
kuwashangilia mashujaa hao, ambao walifanikiwa kushika nafasi ya pili nyuma ya
Kenya ambao ndio walikuwa Mabingwa.
(c )
Disemba 23, 2017 ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa timu ya mpira wa miguu ya Taifa ya
Zanzibar,’Zanzibar Heroes’ baada ya Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwazawadia
viwanja vya kujenga nyumba pamoja na fedha taslim Shilingi milioni tatu kwa
kila mchezaji na kiongozi wa timu hiyo.
Zawadi hizo
alizitowa katika tafrija maalum iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi la zamani Kikwajuni mjini Zanzibar sambamba na taarab maalum
aliyowaandalia timu hiyo iliyotumbuizwa
na kikundi cha Taifa cha Taarab cha Zanzibar kufuatia kufanya vizuri
katika mashindano ya mwaka huu ya Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati
‘CECAFA’ na kupata nafasi ya pili.
Dk. Shein alitoa
zawadi hiyo kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa siku moja kabla katika viwanja
vya Ikulu mjini Zanzibar ambapo akitoa salamu zake na pongezi kwa wachezaji na
viongozi wa timu hiyo alikataa kuzitaja zawadi hizo na ambazo jumla yake
zilikuwa tatu na aliitaja ile ya taaraab tu na kusema mbili angezitaja
siku hiyo.
Vigeregere, hoihoi
na nderemo zilisikika katika ukumbi huo kutoka kwa wachezaji na viongozi wa
timu hiyo pamoja na hadhara iliyohudhuria tafrija hiyo mara baada ya Rais Dk.
Shein kuzitangaza zawadi hizo ambazo kila mmoja alikuwa anasubiri kwa hamu
kuzisikia.
Rais Dk. Shein
aliwakabidhi hundi ya Shilingi za Kitanzania milioni tatu kwa kila mchezaji na
viongozi ambao kwa ujumla wao ni 33 huku akiwaeleza kuwa kwa upande wa viwanja
watakabidhiwa si muda mrefu baada ya kukamilika hati zao na nyaraka nyengine
muhimu kutoka kwa Wizara husika ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.
9. ZU KUBEBA KOMBE LA VYUO VIKUU TANZANIA
Disemba 20, 2017 Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha
Zanzibar University (ZU) ilifanikiwa kutwaa kombe kwenye mashindano ya Vyuo
Vikuu vya Tanzania (TUSA CUP) baada ya kuichapa Chuo cha St John cha Dodoma 4-0
mchezo iliopigwa huko Dodoma.
10.
ZANZIBAR SAND HEROES KUSHINDA TAJI LA COPA DAR ES SALAM
Disemba 26, 2017 timu ya Taifa ya Zanzibar kwa
upande wa soka la Ufukweni (Zanzibar Sand Heroes) ilitwaa kombe la Copa Dar es
salam baada ya kuifunga Malawi mabao 3-2 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa
kwenye fukwe za Coco.
Comments
Post a Comment