ZANZIBAR HEROES WAANZA KUFURAHISHWA NA DK SHEIN, LEO WAITWA IKULU KESHO WANAPEWA SHAVU JENGINE
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameendelea kutoa pongezi kwa timu ya Taifa ya
Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’ kwa kuirudishia Zanzibar heshima yake na sasa
imekuwa inasemwa vizuri kutokana na jinsi timu hiyo ilivyoonesha kiwango safi
cha kusakata soka.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar katika chakula
maalum cha mchana alichowaandalia wachezaji wa Timu ya Zanzibar Heroes pamoja
na viongozi wake wote baada ya kufanya vyema katika mashindano ya mwaka huu ya
Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ yaliofanyika nchini Kenya.
Katika hotuba
yake fupi kwenye hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa
Serikali,akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, viongozi wa ZFA na
waalikwa wengine, Dk. Shein alieleza kuwa vijana hao wa ‘Zanzibar Heroes’
pamoja na kocha wao mkuu wa timu hiyo wamefanya kazi nzuri na ya kupongeza
hatua ambayo itaendelea kuipa heshima kubwa Zanzibar.
Aliongeza kuwa
wachezaji hao wa ‘Zanzibar Heroes’ wamewanawa uso Wazanzibari wote kutokana na
uwezo na nguvu ya mpira waliouonesha na hadi kufikia fainali za mashindano hayo
ya CECAFA.
Dk. Shein
alieleza kuwa watu waliowengi hawakuifikiria timu hiyo ya Zanzibar kama itafika
ilipofika na pia baadhi ya watu hawakuwa wakiisema vizuri lakini hatimae
imedhihirisha kuwa Zanzibar ina historia nzuri ya soka na kuondosha usemi kuwa
‘Chenga twawala’.
“Lazima watambue
kuwa wakiona vyaelea wajue kama vimeundwa kwani wachezaji wetu hawa wamefanya kazi
kubwa na wameiletea heshima kubwa Zanzibar na hivi sasa Zanzibar inasemwa
vizuri kunzia tarehe 17 hadi leo”,alisema Dk. Shein.
“Watu walikuwa
wanaulizana ndio wale hawa tunaowajua au... kocha mkuu hajatuambia siri yake na
wala asituambie kwani amefanya kazi kubwa”,alisema Dk. Shein.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa haikuwa bahati kwa timu hiyo ya Zanzibar Heroes kupata kombe la
ushindi wa mwanzo lakini jitihada kubwa walizifanya wachezaji hao na
kuwapelekea Wazanzibar na Watanzania wote kwa jumla kufurahi.
Alieleza kuwa
Zanzibar imeshawahi kuchukua vikombe vingi katika mashindano mengi ya siku za
nyuma tokea kombe la Goseji, hivyo, haikuwa bahati kwa mwaka hu kupata ushindi
huo licha ya juhudi hizo kubwa zilizochukuliwa na vijana hao mahiri.
Dk. Shein ambaye
yeye mwenyewe ni mpenda michezo na aliwahi kuwa mwanamichezo maarufu hapa
nchini hapo siku za nyuma alieleza kuwa hamasa na bidii za wachezaji hao pamoja
na kocha wao mkuu zimesaidia kwa kiasi kikubwa na kuipelekea timu hiyo kuwa
tishio katika mashindano hayo.
Dk. Shein
alieleza jinsi alivyotoa salamu zake za pongezi kwa timu hiyo baada ya kuingia
fainali ya kombe hilo na baada ya kumalizika kwa mashindano hayo na hatimae
timu hiyo kuibuka kuwa mshindi wa pili.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa kuwaandalia chakula hicho cha mchana hivi leo ni mwanzo tu wa
pongezi zake lakini kuna zawadi tatu kubwa amewaandalia ikianzia taarab maalum
ya kikundi cha Taifa cha Zanzibar pamoja na zawadi nyengine mbili kubwa ambazo
hazijawahi kutokea na kukataa kuzitaja hii leo na kuahidi kuzitaja hapo kesho
atakapozitoa.
“Hii leo ni
bashrafu tu, mchezo kamili utakuwa hapo kesho tukijaaliwa usiku na tumeamua
kufanya hivi kwa mapenzi makubwa na furaha kwa timu yetu hii”,alisema Dk. Shein
huku akisisitiza kuwa taarab hiyo ya kikundi cha Taifa huwa ni taarab maalum
kwa watu maalum na kwa wakati maalum.
Nae Kocha Mkuu wa
Zanzibar Heroes Hemed Suleiman Moroko alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja
na kwa viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kocha Abdulkhani
Msoma pamoja na Mwalimu Abdalla Mwinyi kutokana na nasaha zake za kutaka
wachezaji wawe na silka na hulka za Kizanzibari wakiwa katika mashindano hayo
ambazo ndizo zilizowasaidia.
Moroko aliongeza
kuwa kilichompa ari ya ushindi huo walioupata ni kutokana na kuwa anajua Rais
wa Zanzibar amecheza mpira na anaujua mpira hivyo alihakikisha kuwa hamuangushi
Rais pamoja na Wazanzibari wote.
Pamoja na hayo,
Kocha mkuu huyo alitoa ombi maalum kwa Rais Dk. Shein kumualika Rais wa
Shirikisho la Soka Barani Afrika Ahmad Ahmad kuja Zanzibar ili kufanya
mazungumzo nae kwa ajili ya kuzungumza mustakbali wa Zanzibar katika soka
kimataifa.
Timu ya mpira wa
miguu ya Zanzibar Heroes imefanikiwa kushika
nafasi ya pili ya michuano hiyo ya ‘CECAFA’ baada ya kupata matokeo ya kufungwa
magoli 3-2 kwa changamoto ya mikwaju ya penanti baada ya kwenda sare ya goli
2-2 kwa dakika 12 na timu ya Taifa ya Kenya.
Baada ya matokeo
na ushindi huo sambamba na juhudi kubwa zilizofanywa na timu hiyo, mapokezi
makubwa ya kihistoria yalifanywa hapa Zanzibar na wananchi kutoka maeneo mbali
mbali waliipokea timu hiyo huku pongezi kutoka kwa viongozi na wananchi
zikitolewa, ambapo Dk. Shein akiwa Mkoani Dodoma alitoa pongezi zake kwa timu
hiyo na hvi leo amewaandalia chakula cha mchana na kesho atawaandalia tafrija
maalum itakayoendana na Taarab ya kikundi cha Taifa cha Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Comments
Post a Comment