BALOZI SEIF AHIMIZA MAZOEZI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema kwamba Jamii inapaswa kuzingatia ulazima wa kufanya mazoezi ya Viungo
kila mara ili iweze kujenga afya njema na hatimae kupunguza gharama za matibabu
kwa magonjwa yanayoweza kutibika.
Alisema kulingana na mabadiliko ya mifumo ya Afya na
Ulaji wa vyakula vya kutengeneza visivyozingatia utaratibu wa Kitaalamu Duniani
kote mazoezi yanalazimika kupewa kipaumbele kikubwa katika kuimarisha Afya za
Wanaadamu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mapema asubuhi wakati
wa Bonaza la Vikundi vya Mazoezi Nchini lililoandaliwa
na kikundi cha New Life Exercise Club na kile cha Kiembe Samaki Fitness Club na
kufanyika katika Uwanja wa Amaan Mjini zanzibar.
Alisema mazoezi ni sehemu pia inayowafanya Watu kuondokana na mihemko na
kuachana na mawazo ya kufanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Hivyo
ametoa wito kwa wanamichezo hao kuwa Mabalozi wa Kampeni ya kuwahimiza watu
wafanye mazoezi, kupinga udhalilishaji, kuchangia damu pamoja na kupiga vita
dawa za kulevya.
“ Napenda nisisitize kuwa mazoezi kama hayo yatumike
katika kuhamasisha Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla ili waweze
kuepukana na maradhi tofauti”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alielezea kwamba anatambua changamoto
zinazovikabili vikundi vya mazoezi Nchini lakini bado wako pamoja na Serikali
yao katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kuhamasisha watu kufanya mazoezi
sambamba na kuchangia damu jambo ambalo
ni muhimu katika kuokoa maisha ya Watu.
Alitoa wito kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo kushirikiana na Uongozi wa Vikundi vya Mazoezi katika kuona
changamoto ndogo ndogo zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi.
Balozi Seif alisema ni vyema ushiriki wa sehemu hizo
mbili ukasaidia jinsi ya kuboresha mazoezi hasa kwa kuvipatia Elimu Vikundi vya
Mazoezi ili wanamichezo wao waweze kwenda na wakati kwa kufanya mazoezi yenye
tija kwa Afya zao.
Balozi Seif aliwapongeza Viongozi wa Vikundi vya New
Life Exercise Club na Kiembe Samaki Fitness Club kwa jitihada zao katika
kuwaunganisha na kuwaweka pamoja wana vikundi vya mazoezi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasisitiza
wanavikundi na wanamichezo pamoja na mazoezi wanayofanya, wasiache kupima afya
zao kila mara ambako kunaweza kusaidia kuepusha vifo vya Ghafla.
“ Kupima Afya ni muhimu sana, hasa Virusi vya
Ukimwi, kisukari, maradhi ya Moyo, tezi dume kwa wale wenye umri ulipindukia wa
Miaka 55. Kuna maradhi yakigundulika mapema yanatibika”. Alisema Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema jamii imeshuhudia mara nyingi
kuona vifo vya ghafla vinavyotokea Mitaani ambavyo historia yake inapogundulika
hubaini kwamba marehemu hakuwa na tabia ya kupima afya pengine alikuwa na
ugonjwa kwa muda mrefu usiojuilikana mapema.
Akitoma Risala mwakilishi wa Vikundi vya mazoezi vya
New Life Exercise Club, Kiembe Samaki Fitness Club na Hits FM Kudra Mawazo
alisema Bonaza hilo lililoasisiwa Mwezi Disemba Mwaka 2017 limebeba
dhana nzima ya Kampeni Maalum ya kupinga udhalilishaji wa Kijinsia unaoonekana
kushamiri katika Mitaa mbali mbali Nchini.
Kudra alisema Siku 16 zilizotengwa Maalum kwa ajili
ya Kampeni hiyo zimesaidia kuwaunganisha Wanamichezo katika pembe zote za Zanzibar
kujenga Uzalendo unaosaidia kuunganisha
nguvu za kukabiliana pia na Dawa za Kulevya Visiwani Zanzibar.
Hata hivyo
Kudra Mawazo alielezea changamoto kadhaa zinazovikabili Vikundi mbali mbali vya
Mazoezi Nchini akizitaja baadhi kuwa ni kufanya mazoezi katika Viwanja vya
kukodi pamoja na ukosefu wa Vifaa na Jezi za mazoezi.
Mapema Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed
Mahmoud alisema Kampeni Maalum ya
kupinga udhalilishaji wa Kijinsia iliyoanza kuchanja mbuga mara baada ya Dua ya
kuliombea Taifa kuwa na Amani Mwezi Disemba Mwaka 2016 imeanza kufahamika
miongoni mwa Wananchi.
Alisema Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi inaendelea
kuchukuwa hatua za kupinga udhalilishaji zinazoibuka na kuhusisha zaidi vyanzo vya
maeneo ya Starehe kama Baa, Miziki ya usiku pamoja na michezo isiyozingatia
Maadili na Tamaduni za Taifa.
Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi alionya na
kutahadharisha wazi kwamba Serikali haitamuonea haya au kumuogopa Mtu ye yote
kwa sababu ya Umaarufu, cheo au Ujanja atakaotumia katika kufanya vitendo vya
kudhalilisha Watu hasa Wanawake na Watoto wasiyo na hatia ye yote.
Ayoub aliahidi kuwa Serikali kupitia vyombo vyake
vya Dola itaendelea kulinda raia zake
wote katika misingi ya usawa pamoja na kuwaepusha na changamoto za vitendo
vyovyote vilivyo nje ya maadili, Sheria na Taratibu zilizowekwa.
Mapema asubuhi Wanamichezo hao kutoka Vikundi mbali
mbali Mjini na Vijijini walifanya Matembezi yaliyoanzia viwanja vya Komba
Wapya, kwa kupitia Biziredi, Muambe Ladu, Mikunguni, Kwawazee na kushia Uwanja wa Amaan.
Katika Bonaza hilo liloshirikisha michezo mbali
mbali ukiwemo ule maarufu wa kuvuta Kamba pamoja naUmahiri mkubwa uliyoonyeshwa
na Binti Mdogo wa Miaka 10 Ahlan Saleh kwa kucheza Mchezo wa Yoga.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/2/2018.
Comments
Post a Comment