ZESCO UNITED YAWASILI ZANZIBAR, TAYARI KUWAVAA JKU JUMAMOSI
Wapinzani wa JKU katika
michuano ya Klabu Bingwa Afrika timu ya Zesco United kutoka Zambia wamewasili leo
Zanzibar tayari kabisa kwa mchezo wa Jumamosi kwenye uwanja wa Amaan.
Timu hiyo imewasili leo saa nne asubuhi kwenye uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kwa ndege ya Shirika la Ndege la
Kenya ambapo wachezaji wa timu hiyo wameongozana na viongozi wao na
wamepokelewa na wenyeji wao ambao ni viongozi wa timu ya JKU.
Afisa habari wa chama cha soka Zanzibar (ZFA) Ali
Bakar (Cheupe) amesema kwa upande wao Chama maandalizi yote wamekamilisha huku
akiwataka Mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kwenda kuzishangiria timu za
Zanzibar.
Wawakilishi wa Zanzibar katika Mashindano hayo ya
Kimataifa ni JKU ambao wataivaa Zesco United siku ya Jumamosi katika mchezo wa
kombe la Klabu bingwa huku Zimamoto ambao watawakilisha kwenye kombe la
Shirikisho wataivaa Walaitta Dicha ya Ethiopia siku ya Jumapili michezo yote
itapigwa majira ya saa 10:00 za jioni katika uwanja wa Amaan.
Comments
Post a Comment