TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU TIMU YA KARUME BOYS ITATOLEWA KESHO
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya
Vijana Sanaa Utamaduni na Michezo kesho inatarajia kutoa taarifa na ufafanuzi
juu ya timu yake ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (Karume Boys) ambayo
imeondolewa kwenye Mashindano ya CECAFA U-17 yanayoendelea nchini Burundi.
Karume boys imeondolewa katika Mashindano hayo na kupigwa
faini ya Dola 15000 pamoja na kufungiwa mwaka mmoja kwa kosa la kuorodhesha
wachezaji waliozaliwa kabla ya 01/01/2002.
Katibu mkuu wa Wizara hiyo Omar Hassan (King) atatoa taarifa
na ufafanuzi punde kesho majira ya Mchana katika ukumbi wa Wizara ya Habari
Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Mjini Unguja ambapo Wizara hiyo itapokea
Barua kutoka Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) .
Karume boys ilikuwa icheze jana mchezo wake wa kwanza dhidi
ya Sudan katika uwanja wa Gitega mchezo ambao haukuchezwa baada ya Sudan kupeleka
malalamiko yao kwa CECAFA na mchezo huo ukafutwa.
Wakati huo huo katika kundi A Ethiopia imenyanganywa ushindi dhidi ya Somalia kwasababu ya
kuwachezesha wachezaji watatu waliozidi umri ambapo wachezaji hao watarejeshwa
kwao kesho Jumanne.
Hivyo Wazanzibar kwa ujumla wasubiri taarifa ya Wizara kuhusu
ufafanuzi wa tukio hilo na si kuongea na kutuma vitu vilivyokuwa havina uhakika
bila ya kujua usahihi na ukweli wake.
Comments
Post a Comment