RAIS WA ZFA AJIUZULU RASMI
Rais wa ZFA wa Kati kati Ravia Idarous Faina |
Rais wa Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) Ravia Idarous
Faina ameandika barua rasmi ya kujiuzulu nafasi yake na sasa wataungana na
Makamo wa Urais ZFA Unguja Mzee Zam Ali na Mkurugenzi wa ufundi Abdulghan Msoma
ambao walitangaza kujiuzulu mwishoni mwa mwezi Mei, 2018.
Katibu mkuu wa ZFA Mohammed Ali Hilali (Tedy) amethibitisha
kupokea barua hiyo ya Ravia.
“Ni kweli ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake, barua
ameileta leo Jumatano saa 9 za mchana”. Alisema Tedy.
Ravia alipokea kijiti hicho cha Urais kutoka kwa Amani Ibrahim
Makungu mwaka 2013.
Yote hayo inawezekana ikawa sababu kufuatia Zanzibar kupitia
timu yake ya Vijana ya Karume Boys kuondolewa katika Mashindano ya Cecafa ya
Vijana yaliyofanyika hivi karibuni nchini Burundi ambapo Karume Boys licha ya
kuondoshwa katika Mashindano pia walipigwa faini kwa kosa la kuorodhesha
wachezaji waliozaliwa kabla ya 01/01/2002 ambapo walikwenda kinyume na kanuni
ya Mashindano.
Kutokana na makosa hayo Karume boys imepewa adahabu tatu
ikiwemo kuondolewa mashindanoni, inaambatana na faini dola 15,000 (Sh 30
milioni) zinazotakiwa kulipwa na Chama cha Soka la Zanzibar (ZFA), ambapo fedha
hizo zitafidia gharama za tiketi, malazi na chakula ya timu katika kipindi
chote walichokaa Burundi huku adhabu ya tatu ikiwa kufungiwa kutoshiriki
mashindano yanayoendeshwa na CECAFA hadi hapo watakapolipa faini hiyo ambayo
inatakiwa kurudishwa FIFA.
Comments
Post a Comment