RAZA AUTAKA URAIS WA ZFA, ATANGAZA RASMI NIA
Mwakilishi wa jimbo la Uzini Mohammedraza Hassanal
ametangaza nia ya kugombea Urais wa Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kwa
ajili ya kuliteka maendeleo ya mchezo huo.
Raza ameyasema
hayo wakati akizungumza na wandishi wa habari za michezo katika hafla maalum iliyofanyika
katika ukumbi wa hotel ya Golden Tulip Malindi Mjini Unguja.
Mwanamichezo huyo
ambae aliwahi kuwa mshauri wa masuala ya michezo kwa Rais wa awamu ya tano Dk
Salmin Amour, amesema nia hiyo imekuja baada ya kuona soka la Zanzibar
kuanguka, hivyo ameona ipo haja kutangaza nia ili kuja kulikomboa.
Amesema
atahakikisha anaukuza mchezo huo kwani atashirikiana ipasavyo na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inaonekana ipo mstari wa mbele kwenye michezo.
ZFA watalazimika
kufanya uchaguzi kufuatia viongozi wake wakuu kuamua kujiuzulu akiwemo
aliyekuwa Rais Ravia Idarous Faina, Makamo Urais ZFA Pemba Ali Mohammed Ali na
Makamo Urais ZFA Unguja Mzee Zam Ali hivyo nafasi hizo mpaka sasa zipo tupu
huku ikisubiriwa kamati ya Uchaguzi kutangaza tarehe za kuanza harakati za
kufanyika uchaguzi huo.
Comments
Post a Comment