RIADHA NOMA ZANZIBAR, WATINGA FAINALI,SOKA KIKAPU, MIKONO, MEZA KAMA KAWAIDA WATESA
Kikosi cha Mpira wa Kikapu kanda ya Unguja |
MASHINDANO ya Umisseta yanazidi kushika kasi hapa Mwanza,
huku timu ya kanda ya Pemba na Unguja zikiendelea kufanya vyema kwa baadhi ya
michezo.
Katika michezo iliyochezwa leo nyakati za asubuhi, mchana na
jioni, timu ya riadha Kanda ya Unguja imeweza kutinga hatua ya fainali baada ya
kutamba kwenye mbio za mita 100 wanaume na wanawake, ambapo walioshinda ni
wanaume ni Mohamed Rashid na Omar Rashid, wanawake ni Naima Ali na Nasra
Abdalla Abdalla.
Lakini kanda ya Pemba kwa upande wa riadha haikufanya vyema
baada ya wakimbiaji wake kushindwa kuingia hatua ya fainali kwenye mbio za mita
100 , wakati mbio za mita 400 iliweza kushika nafasi ya nne na sita katika
makundi yao.
Wakati huo huo kanda
ya Unguja imeweza kutoka na ushindi katika mchezo wa mpira wa kikapu ambapo
ilicheza michezo miwili tofauti.
Mchezo wa kwanza iliweza kutoka na ushindi wa vikapu 62-13 dhidi ya mkoa wa Njombe, wakati
mchezo wa pili Unguja iliishinda mkoa wa Mtwara kwa vikapu 24-23.
Mchezo wa mpira wa mikono Unguja iliweza kutoka na ushindi
wa mabao 25-12 dhidi ya mkoa wa Njombe, pambano ambalo Unguja ilitawala zaidi
kipindi cha kwanza, lakini ikapunguza kasi kipindi cha pili na kuwapa nafsi
wapinzani kupata mabao.
Mpira wa netiboli timu Unguja imeendelea kuchemsha katika
michezo yake, baada ya kupokea kichapo cha mabao 42-31 kutoka kwa mkoa wa Mara,
matokeo ambayo yanaiweka nafasi finyu Unguja kuweza kuiongia hatua ya robo
fainali.
Lakini pia kanda ya Unguja imeweza kufanya vyema katika
mchezo wa mpira wa Meza (Table tennis), ambapo michezo miwili ilipigwa, mchezo
wa kwanza mchezaji Sultani Suleiman alishinda kwa seti 2-1 dhidi ya Mkoa wa
Manyara, wakati mchezo wa pili Mwanajuma Bakar alishinda kwa seti 2-0 dhidi ya
Manyara.
Mpira wa mchezo wa Wavu Unguja ikaendelea kufanya vibaya
baada ya kufungwa tena seti 3-0 na mkoa wa Mara, hivyo hadi sasa kupoteza
michezo mitatu.
Kwa upande wa soka timu ya Pemba imefanikiwa kuwachapa Dodoma
1-0 huku ikiendelea kuongoza kundi lake B kwa kujikusanyia alama 12 baada ya
kushinda michezo minne na kupoteza mchezo mmoja.
Comments
Post a Comment