ZANZIBAR YAZIDI KUNG’ARA UMISSETA, INAONGOZA MAKUNDI YAO
TIMU za Zanzibar zimeendelea kufanya vyema katika
michezo yake mbali mbali iliyocheza leo, baada ya kuibuka na ushindi na kuleta matumaini
makubwa ya kuingia hatua ya robo fainali kwenye Mashindano ya Michezo na Sanaa
kwa Skuli za Sekondari Tanzania (UMISSETA) yanoyoendelea katika Viwanja vya
Chuo cha Ualimu Butimba, Mwanza.
Katika michezo iliyopigwa leo, upande wa Soka timu
ya Unguja imefanikiwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi Morogoro, mchezo ambao
ulikuwa mkali na kuvutia kwa muda wote.
Katika pambano hilo, licha ya kufungwa Morogoro
walionesha kiwango kizuri na kuwabana Unguja ambapo hadi kipindi cha kwanza
kinamalizika cha hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi na nguvu mpya
kila mmoja akitaka kupata bao la mapema, lakini bahati hiyo iliwaangukia Unguja
baada ya kuandika bao hilo pekee lililokwamishwa wavuni dakika ya 72 kupitia
kwa Ali Hassan (Ndimbo).
Mchezo mwengine uliwakutanisha kanda ya Pemba ambayo
ilikuwa na kazi ya kupepetena na mkoa wa Singida, pambano ambalo lilimalizika
kwa Pemba kuibuka na ushindi wa bao1-0 dhidi ya Singida bao ambalo lilifungwa
na mchezaji Mohamed Ali ndani ya dakika ya 15.
Kwa upande wa mchezo wa mpira wa Mikono (Handball) timu
ya kanda ya Unguja imefanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 22-2 dhidi ya
Mtwara.
Kumalizika kwa michezo hiyo tumezungumza na captain
wa soka Unguja Ibrahim Ali (Chafu) na wa Pemba Abdul latif Said Masoud wamesema
kutokana na maandalizi waliyoyafanya wataendelea kutesa kwenye Mashindano hayo.
Timu ya Soka ya Kanda ya Pemba inaongoza kundi lao B
wakiwa na alama 9 baada ya kushinda michezo yote mitatu kufuatia mchezo wa
awali kuwafunga Mabingwa watetezi Songwe 1-0, kisha jana kuwachapa Shinyanga bao
1-0 na leo kuwamaliza Singida 1-0 hivyo wamecheza michezo mitatu mfululizo bila
ya lango lao kuruhusu kufungwa hata bao moja.
Unguja wao wapo kundi D wanaongoza pia kufuatia
kushinda yote miwili na kuwa na alama sita baada ya mchezo wa kwanza kuwafunga Mtwara
mabao 2-1 na leo kuwachapa Morogoro bao 1-0 ambapo kesho saa 2:00 za asubuhi
watakuwa na mchezo wao watatu kucheza na Njombe.
Comments
Post a Comment