MKOA WA KUSINI UNGUJA TISHIO TFF CUP U-17
Kikosi cha Mkoa wa Kusini Unguja Timu ya Mkoa wa Kusini Unguja imeendeleza wimbi lake la ushindi baada ya kushinda michezo miwili mfululizo ya mwanzo kufuatia asubuhi ya leo kufanikiwa kuifunga timu ya Mkoa wa Mbeya mabao 2-1 kwenye Mashindano ya TFF ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi. Katika mchezo huo timu ya Mbeya ilitangulia kupata bao dakika ya 43 kipindi cha kwanza kwa bao la Bernard Peter lakini Kusini wakajipanga upya kipindi cha pili kwa kusawazisha na kuongeza bao kwenye dakika ya 55 na 70 kwa Mabao Ramadhan Mwita Haji na Hafidh Othman Kombo. Huu ni ushindi wa Pili kwa Mkoa wa Kusini Unguja kufuatia mchezo wa kwanza kuifunga Lindi bao 1-0 ambapo sasa ina alama 6 na kuongoza kundi lao B. Wawakilishi wengine wa Zanzibar kwenye Mashindano hayo timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi leo imejikuta ikipoteza baada ya kufungwa na Mkoa wa Songwe mabao 2-1 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Kibaha.