ATTAI NA HUSSEIN WACHINJWA NA ZFA, WAFUNGIWA MAISHA KUTOJIHUSISHA NA SOKA
![]() |
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA, Mkutano uliofanyika leo Gombani Pemba |
Mkutano Mkuu wa dharura wa Chama cha Soka Visiwani Zanzibar “ZFA”
umewafukuza wajumbe wake wawili Hussen Ali Ahmada na Massoud Attai na
kuwafungia maisha kutojihusisha na Soka kutokana na sababu tofauti.
Maamuzi hayo yameamuliwa katika Mkutano huo wa dharura
uliofanyika asubuhi ya leo katika Ukumbi wa Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba.
Akizungumza na Mtandao mara baada ya kumalizika Mkutano huo
Ali Bakar “Cheupe” ambae ni Afisa habari wa ZFA amesema sababu zilizopelekea kufukuzwa
wawili hao ni kukiuka Maadili ya ZFA na ndio mana wamewatimua kwenye chama
chao.
“Mkutano Mkuu leo umeamua kuwafungia maisha kutojishughulisha
na soka wajumbe wetu wawili Attai na Hussein, sababu kubwa kwa Hussein yeye alitumia
vibaya madaraka wakati ule soka lilikuwa linaongozwa na kamati ya muda na yeye
ndie aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, lakini kwa upande wake Attai yeye
alifanya ubadhilifu wa Fedha na pia alituhumiwa kuviibia vilabu ambavyo
viliingia katika Mashindano ya Kimataifa zikiwemo Polisi, KMKM, Mafunzo na JKU
ambapo fedha alipewa yeye na kule CAF hajazipeleka”. Alisema Cheupe.
Attai alikuwa ni mjumbe wa ZFA Wilaya ya Kaskazini “A” kwenda
Taifa huku Hussein yeye alikuwa ni Mjumbe ZFA Wilaya ya Mjini kwenda Taifa
ambapo kwasasa Wilaya hizo zinatarajia kufanya Uchaguzi kwa haraka huku Wilaya
ya Mjini huwenda ikafanya April 30, 2017.
Comments
Post a Comment