KAMATI YA KATIBA YA ZFA YAWATOWA HOFU WAZANZIBAR KUHUSU KATIBA WATAKAYOIREKEBISHA KUENDANA NA MATAKWA YA CAF


Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuifanyia marekebisho katiba ZFA ili kuendana na matakwa ya Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” inatarajia kuiwasilisha rasimu ya awali ya katiba kwa takribani wiki mbili kwa Chama cha Soka Zanzibar “ZFA”.

Akizungumza na kisanduzenj.blogspot.com katibu wa kamati hiyo Saleh Ali Said ambae pia ni Mwanasheria wa ZFA amesema wameanza kazi za kuandaa katiba hiyo ambapo jana Jumamosi wameanza kazi ya awali na zoezi hilo litachukua muda mfupi tu kukamilika.

“Tushaanza kazi hiyo mana tumekutana wajumbe na zoezi hili si kubwa sana, tutachukua wiki moja na nusu au mbili tu kukamilisha rasimu ya awali ya katiba kisha tutaiwasilisha kwa ZFA, Wazanzibar wasiwe na hofu katiba hiyo itakuwa inaendana na matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika pamoja na kwa maslahi ya Mazingira ya Visiwa vya Zanzibar”. Alisema Saleh.

Awali Kamati hiyo ilihitaji fedha kwaajili ya bajeti yao ili kufanikisha zoezi hilo ambapo ilihitaji jumla ni shs Milioni thalasini na tisa , laki nane na hamsini elfu (39,850,000/=) lakini zoezi hilo likashindwa kufanyika kutokana na ZFA kushindwa kuwapatia fedha hizo ambapo kwasasa wameweka uzalendo mbele na kukubali kufanya kazi hiyo bila ya fedha hizo baada ya ZFA kupatiwa uanachama wa kudumu wa CAF sasa zoezi hilo litakuwa rahisi mno kuliko awali kwani katiba inayotakiwa iendane na matakwa ya CAF.

Viongozi sita (6) waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Afan Othman Juma (Mwenyekiti), Saleh Ali Said (Katibu), Othman Ali Hamad (Msaidizi Katibu), pia yumo Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka la Wanawake (Zanzibar Queens) Nassra Juma na wengine ni Eliud Peter Mvella na Ame Abdallah  Dunia.
Saleh Ali Said Mwanasheria wa ZFA

Comments

Popular posts from this blog

HUYU NDIYE MCHEZAJI MWENYE REKODI YA KUFUNGA MAGOLI MENGI KWENYE MECHI YA TAIFA DHIDI YA BOYS