KOCHA WA ZANZIBAR HEROES AREJEA ZENJ AKITOKA CAMEROON KWENYE KOZI YA CAF YA MAGOLIKIPA
Kocha wa Makipa wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar
Heroes) ambae pia ni kocha Mkuu wa timu ya Malindi Saleh Ahmed Seif “Machupa” amerejea
Visiwani Zanzibar akitokea Cameroon kwenye Kozi ya CAF ya Wakufunzi wa Makocha
wa Magolikipa iliomaliza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika kozi hiyo ya Wakufunzi wa Makocha wa Magolikipa iliyofanyika
wiki moja huko Cameroon Machupa amefanikiwa kuhitimu vyema na sasa atakuwa
Mkufunzi rasmi wa Makocha wa Magolikipa Zanzibar.
Mara baada ya kuwasili tu visiwani Zanzibar Blog ya kisanduzenj.blogspot.com
imefanikiwa kumnasa kocha huyo na akielezea kozi hiyo ilivyokuwa.
“Kozi ilikuwa si nyepese lakini nashkuru kumaliza salama na
kufanikiwa, hivyo sasa nimefanikiwa kuwa Mkufunzi rasmi wa Makocha wa
Magolikipa ndani ya nchi yangu, Wakufunzi wengine wanasomesha nchi yoyote
Afrika lakini mimi kiwango changu cha awali natakiwa kusomesha Zanzibar, hivyo
kwa msimu ujao makocha wa Magolikipa wanatakiwa wawe na japo kozi ya Msingi
wakikaa kwenye benchi ndani ya ligi kuu, hivyo nawaomba makocha wenzangu
tujiendeleze kusoma pindi tunaposikia nafasi zimetoka kwani huko mbele
tunapokwenda ni kugumu mno, na mimi natarajia kuendesha hiyo kozi”. Alisema
Machupa.
Mbali ya kuhitimu kuwa Mkufunzi wa ndani, Machupa pia ameshahitimu
kozi ya FIFA ya Ukocha wa Magolikipa ya hatua ya juu (Advanced Level) ambayo
aliipata kwenye kozi iliyofayika tarehe 01 Agost, 2016 na kumalizika tarehe 05
Agost 2016, na pia Machupa ana Leseni “B” ya Ukocha inayotambuliwa na CAF.
Comments
Post a Comment