MAKOCHA WATANGAZIWA AJIRA TIMU ZA TAIFA ZA VIJANA ZANZIBAR, WATAKIWA KUOMBA NAFASI HIZO
Kamati ya Makocha wa Soka Visiwani Zanzibar ambayo imepewa
dhamana na ZFA ya kuteuwa Makocha wa timu za Taifa za Vijana imetangaza nafasi
za Makocha wanohitaji kuwa makocha wa timu za Taifa za Vijana Zanzibar chini ya
umri wa miaka 14, 17 na 20 ambapo wametakiwa kwenda kuchukua fomu ya kuomba
maombi hayo.
Akizungumza na Mtandao huu Katibu wa Kamati ya Makocha
Visiwani Zanzibar Ibrahim Makeresa amesema kocha yeyote anaehitaji kuwa kocha
mkuu au msaidizi wa timu hizo za vijana kwenda Afisini kwao kuchukua fomu na
ikiwa atakidhi vigezo atapewa nafasi hiyo.
Ameelezea lengo la kutoa fomu maalum kwa makocha hao ni
kuondoa malalamiko kwa baadhi ya wadau ambao mara nyingi wanalalamika kuwa
makocha wa timu hizo wanateuliwa kwa upendeleo, ambapo amesisitiza kuwa mwenye
sifa aombe kisha watachaguliwa kwa kuepusha malalamiko hayo.
“Unajua miaka ya nyuma akitangazwa kocha wa timu za vijana
kuna kuja maneno mengi kwamba labda nafasi hizo zinakwenda kwa watu maalum,
sasa kwa kuepusha hayo tutatoa fomu maalum kisha makocha waombe na akikidhi
vigezo atachaguliwa ikiwa kocha mkuu au msaidizi”. Alisema Makeresa.
Fomu hizo za kuombea nafasi za ukocha kwa timu za Vijana zinatarajiwa
kuanza kutolewa kuanzia Alhamis ya Mei 25, 2017 na mwisho wa kuzipitia fomu
hizo itakuwa June 5, 2017 ambapo sifa kubwa ya kuwa kocha wa timu hizo, kocha
anatakiwa kuwa na sifa ya ukocha kuanzia Leseni “C” ambayo inayotambuliwa na
shirikisho la soka Barani Afrika na pia sifa nyengine kocha anatakiwa awe
hajapatikana na hatia ya udhalilishaji kwa watoto (Wachezaji).
Comments
Post a Comment