TAARIFA KWA TIMU 28 KUKUTANA KUPATA TIMU 12 ZA LIGI KUU MSIMU MPYA ZITATOLEWA JUMATATU NA ZFA
Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) kinatarajia kutoa
taarifa Jumatatu ya June 19, 2017 ya kutaja tarehe ya kukutana timu 28 ambazo
zitapendekeza mfumo gani utumike ili zipatikane timu 12 za ligi kuu soka ya
Zanzibar za msimu ujao wa mwaka 2017-2018.
Tarehe hiyo ya kukutana vilabu hivyo 28 itatolewa siku hiyo
ya Jumatatu majira ya saa 7:30 za mchana kwenye Afisi za ZFA zilizopo Amani
Mjini Unguja.
Siku ya Alhamis Machi 16, 2017 itaendelea kukumbukwa na Wazanzibar baada ya ZFA
kuingizwa rasmi kuwa Mwanachama wa 55 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF”
kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo kilichofanyika Addis
Ababa nchini Ethiopia.
Moja ya maagizo ya CAF ni kutaka msimu ujao wa mwaka
2017-2018 ligi kuu soka ya Zanzibar iwe na jumla ya timu 12 kwa Zanzibar nzima
ambapo katika msimu huo wa mwaka 2016-2017 ulikuwa na jumla ya timu 36 kwa kila
kanda ilikuwa ina timu 18, yani Kanda ya Unguja 18 na Kanda ya Pemba 18, huku
zimeshashuka timu 12 kati ya hizo 36 kwa kila kanda zimeshuka timu sita (6).
Lakini Wadau wengi wa soka Visiwani Zanzibar wanahamu sana
kujua mfumo gani utatumika kwaajili ya kupatikana timu 12 za ligi kuu soka ya
Zanzibar kwa msimu ujao wa mwaka 2017-2018 ambapo Mkutano Mkuu wa dharura wa
ZFA uliofanyika April 22 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba ulipendekeza
vilabu 28 vya ligi kuu ya Zanzibar vikutane kwa pamoja baada ya kumalizika 8
bora na kupanga ni mfumo gani utumike ili zipatikane timu 12 za msimu mpya.
Timu hizo 28 ni zile ambazo zimenusurika kushuka daraja
katika mkumbo wa awali ambapo zimeshashuka timu 12 kwa kila kanda kushuka 6,
yani Unguja 6 na Pemba 6 pamoja na zile nne za Daraja la Kwanza zilizofanikiwa
kuja juu ambazo ni mbili Unguja na mbili Pemba ndizo zilizofanya kuwa na Jumla
ya timu 28.
Viongozi wa timu hizo 28 za Unguja na Pemba watakutana kwa
pamoja baada ya kutangazwa Jumatatu tarehe hiyo ya kukutana ndipo hapo patajulikana
timu zipi zitacheza ligi kuu msimu ujao na mfumo gani utumike kupatikana kwa
timu hizo 12.
Hivyo pengine mfumo utakaotumika huwenda timu ikawa imefanikiwa
kuwa bingwa au Mshindi wa Pili wa Zanzibar (Wawakilishi wa Klabu Bingwa na
Kombe la Shirikisho) lakini akashindwa kucheza ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu
ujao endapo akishindwa kuvuka katika
mfumo huo ambao utakaotumika.
Comments
Post a Comment