UMISSETA ZANZIBAR WATUA MWANZA, TAYARI KUANZA MASHINDANO KESHO
Msafara wa wanamichezo 135 kutoka Zanzibar
ambao unashiriki mashindano ya
umoja wa Michezo na Sanaa skuli za sekondari Tanzania (UMISSETA) umewasili
Butimba mjini Mwanza tayari kwa mashindano hayo.
Msafara huo uliondoka Zanzibar juzi
Jumamosi Juni 3 na kuwasili Mwanza leo asubuhi
wakiwa katika hali nzuri kiafya, na tayari wameanza kufanya mazoezi madogo kwa ajili ya kuweka miili
yao sawa.
Akizungumza na Mtandao huu jijini
hapa, Mkuu wa msafara Abdalla Makame Makame ambaye pia ni afisa Elimu Mkoa wa
Kusini Unguja, amesema kuwa licha ya safari refu lakini wanamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kufika salama safari yao hiyo.
‘’Tunashukuru tumefika salama hapa Mwanza, tumepokelewa
vizuri tunachosubiri hivi sasa ni kuanza kwa mashindano, na hapa tumefikia
sehemu nzuri hivyo hatuna hofu yoyote’’. Alisema Makame.
Akizungumza kwa niaba ya makocha wa
michezo kocha awa timu ya mpira wa mikono (handball) Salum Hassan, amesema kuwa
vijana wote wapo katika hali nzuri na wapo tayari kwa mashindano.
Amesema kuwa baada ya kufika jioni leo
wataanza kufanya mazoezi kwa ajili ya kuweka sawa miili yao, na hali ya hewa ni
nzuri haina tofauti sana na hali ya hewa ya nyumbani Zanzibar.
‘’Jioni tutafanya mazoezi leo na kesho
tunasubiri ratiba ili tujuwe tumepangwa na nani, lakini kiujumla timu zote zipo
vizuri na hali ya hewa ya hapa haina tofauti kubwa sana ila hapa jua ni kali
sana’’.Alisema.
Hivyo amezidi kuwaomba Wazanzibari
kuendelea kuwaombea dua waweze kucheza
vizuri na hatimae kurudi na makombe mengi .
Katika Mashindano hayo ambayo
yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake kesho Jumanne June 6, 2017 huko Butimba
Chuo cha Ualimu Mkoani Mwanza, Zanzibar itakuwa na kanda mbili tofauti Unguja
timu yao na Pemba timu yao, ambapo kanda ya Unguja itakuwa na timu za Soka,
Wavu, Mikono, Riadha, Mpira wa Meza na Kikapu,wakati kanda ya Pemba itakuwa na
timu za Riadha, Wavu, Kikapu na Soka.
Comments
Post a Comment