UWANJA WA MAO KUANZIA KESHO MUDA WOWOTE KUANZA RASMI KUJENGWA, MHADISI AELEZEA SABABU ZA KUCHELEWA KIDOGO
![]() |
Muonekano wa uwanja wa Mao utakavyokuwa baada ya ujenzi |
Tangu Waziri wa Habari
Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar, Rashid Ali Juma awakabidhi Uwanja wa Mao Tse Tung wakandarasi
wa Kichina kampuni ya Zhengtar Group Company Limited kwaajili ya kuujenga
kisasa uwanja huo ambao utajengwa kwa mwaka mmoja na miezi miwili, zoezi hilo
la ujenzi litaanza rasmi wiki hii kuanzia kesho Jumanne kwa mujibu wa wataalamu
wanaosimamia zoezi hilo.
Mtandao wa kisanduzenj.blogspot.com ulimtafuta Mhandisi wa
uwanja huo Ali Mbarouk Juma ambapo ameelezea sababu zilizochelewa kidogo kuanza
rasmi ujenzi wa uwanja huo.
Mbarouk amesema sababu kubwa iliyopelekea kudorora kujengwa
uwanja huo ni mvua ambapo walilazimika kusitisha ujenzi kwa kupisha mvua hizo.
Aidha amesema vikwazo vyengine vilikuwa ni Vibali vya ujenzi
ambavyo kwasasa tayari wameshapata na muda wowote watabandika bango lao la
ujenzi kwenye eneo la uwanja huo.
“Tulikuwa tunasubiria mvua zipite ndipo ujenzi uanze rasmi,
kwasasa mvua tayari zimeshakata muda wowote kutoka sasa utaanza rasmi,
watakaopita katika eneo la uwanja wa Mao wataona bango ambalo litaonyesha kuwa
pana ujenzi wa uwanja, mana ilikuwa kikwazo chengine vibali vya ujenzi
hatujapata lakini kwasasa mambo yapo fresh na ujenzi kuanzia wiki hii muda
wowote unaanza”. Alisema Mbarouk.
Ujenzi huo utakuwa na Viwanja viwili vya mpira wa miguu na
chengine cha michezo ya ndani kama vile Mpira wa Kikapu, Mpira wa Mikono, Mpira
wa Pete na mengineyo.
Katika Viwanja hivyo vya Mpira wa Miguu uwanja mmoja
utakuwepo upande wa Magharibi ambao utakuwa na Jukwaa moja litakalochukuwa
Mashabiki 1500 waliokaa.
Uwanja mwengine wa mpira wa miguu utakuwepo upande wa
Mashariki ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua Mashabiki waliokaa 900 katika
jukwaa moja ambalo litakuwepo katika Uwanja huo.
Viwanja hivyo vitakuwa na taa ambazo zitaweza kuwezesha
kuchezwa michezo hadi usiku.
Uwanja huo utagharimu Shilingi Bilioni 12.5 kwa fedha za
Tanzania ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itatoa Shilingi Bilioni
11.5 huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia zaidi ya Shilingi
Bilioni 1 kati ya hizo Bilioni 12.5 ambazo watalipwa Wakandarasi wa uwanja huo
ambao ni Kampuni ya Zhengtar Group Company Limited ambayo ina uzoefu mkubwa wa
kujenga Viwanja wa Michezo.
![]() |
Uwanja wa Mao ulivyosasa |
Comments
Post a Comment