ZANZIBAR YAKARIBIA KUPATA UANACHAMA WA FIFA, WANAMICHEZO WATAKIWA KUOMBA DUA
Hivi karibuni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeendelea
na jitihada zake za kuhakikisha Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA) wanapata
uanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) baada ya TFF kuiombea ZFA
kuwa Mwanachama wa Shirikisho hilo.
Kamati Tendaji ya Chama cha mpira wa miguu Zanzibar ZFA imekutana
juzi na Wenyeviti na Makatibu wa ZFA
wilaya saba za Unguja chini rais Ravia Idarous Faina kwenye ukumbi wa uwanja wa
Amaan.
Wajumbe wa kikao hicho kilichoitishwa na kiongozi huyo wa juu
wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar waliweza kupokea taarifa mbili muhimu
kutoka kwa rais huyo.
Katika hatua ya kwanza rais Ravia amewasilisha barua
iliyotumwa na TFF kwenda Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA kuhusiana na
maombi ya ZFA ambapo Wajumbe hao walipokea kwa furaha taarifa hiyo.
TFF tayari imeshatuma Barua rasmi FIFA kuhusu suala hilo
lilalosubiriwa kwa hamu na wapenda soka wa Visiwa vya Zanzibar kuwa na uwezo wa
kushiriki moja kwa moja michezo ya Kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho hilo
la Dunia ikiwemo Kombe la Dunia.
Afisa habari wa ZFA Ali Bakar “Cheupe” amesema Wajumbe wa ZFA
wamepokea kwa furaha kubwa taarifa ya maombi hayo ambapo amewataka Wazanzibar
kuzidi kuomba dua ili Zanzibar ipate uanachama kamili wa FIFA.
“Wanzibar nawaomba tuzidi kuomba dua ili tufanikiwe kupata
uanachama wa FIFA, kama walivyoomba tukapata CAF basi tuwe pamoja kwa hili pia”.
Zanzibar iliingia katika kitabu cha historia Siku ya Alhamis
Machi 16, 2017 baada ya ZFA kuingizwa rasmi kuwa Mwanachama wa 55 wa Shirikisho
la Soka Barani Afrika “CAF” kufuatia Kikao cha 39 cha Mkutano Mkuu wa
Shirikisho hilo kilichofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia.
Comments
Post a Comment