CAF YAMPONGEZA MACHUPA KWA KUENDESHA KOZI YA MAKOCHA WA MAGOLIKIPA
Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF” limefurahishwa kwa
kitendo cha Mkufunzi wao wa Makocha wa Magolikipa Saleh Ahmed Seif “Machupa”
kuharakisha kuendesha kozi ya msingi ya Makocha wa Magolikipa Visiwani Zanzibar
na kusema huo ni uzalendo wa hali ya juu kabisa.
Hayo yamesemwa na Makamo wa Urais wa ZFA Unguja, Mzee Zam Ali
wakati anazungumza na Mtandao huu siku chache baada ya kumalizika kwa kozi hiyo
ambayo ilianza Jumatano ya July 5, 2017 na kumalizika Jumanne ya July 11, 2017
katika ukumbi wa uwanja wa Amaan Mjini Unguja ambapo makocha 29 walihitimu kozi
hiyo.
Zam amesema CAF wamefurahishwa mno kusikia Machupa kaendesha
kozi ambapo wamesema katika Wakufunzi wao wote waliyohitimu kozi ya Wakufunzi
wa Makocha wa Magolikipa nchini Cameroon basi Machupa yeye ndio mzalendo namba
moja kuliko wenzake.
“CAF waliposikia Machupa anaendesha kozi wametutumia ujumbe
katika barua pepe yetu ZFA kwa kumpongeza na kusema kuwa huo ni uzalendo wa
hali ya juu kwa kitendo hicho cha Machupa kwani katika kozi yao waliyosoma kule
Cameroon yeye ndie wa mwanzo kuendesha kozi mapema nchini kwao”. Alisema Zam.
Machupa ni Mkufunzi pekee nchini Tanzania aliyehitimu Kozi ya
CAF ya Wakufunzi wa Makocha wa Magolikipa wa ndani kozi ambayo aliisomea nchini
Cameroon mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Machupa pia ameshahitimu kozi ya
FIFA ya Ukocha wa Magolikipa ya hatua ya juu (Advanced Level) na pia ana Leseni
“B” ya Ukocha inayotambuliwa na CAF.
![]() |
Mkufunzi Saleh Ahmed Seif “Machupa” |
Comments
Post a Comment