MKUFUNZI KUTOKA SWEDEN AWAPIGA MSASA TAEKWON-DO ZANZIBAR
Chama cha mchezo wa Taekwon-do visiwani Zanzibar, kimeandaa
semina maalum ya siku moja kwa wachezaji wa mchezo huo ambapo mkufunzi wa
mafunzo hayo ametoka nchini Sweden.
NIKLAS ENANDER ni mkufunzi anayetambulika na Shirikisho la Taekwon-do
Duniani (ITF) ndie aliyeendesha Mafunzo hayo ya siku moja, Mafunzo ambayo
yamefanyika Jana Amani mjini Unguja katika ukumbi wa Judo kuanzia saa 3:00
asubuhi na kumalizika saa 11:00 za jioni.
NIKLAS amefurahishwa sana kuona idadi ya wachezaji imezidi
tofauti na mwaka jana alipokuja hivyo amezidi kupata moyo wa kuwa karibu na
Wazanzibar.
“Nimefurahi sana kuona Wazanzibar wanapenda michezo, mwaka
jana nilipokuja wachezaji walikuwa kidogo, lakini mwaka huu idadi imeongezeka,
ukweli nimefurahi sana”. Alisema Mkufunzi huyo.
Mchezo wa Taekwon-do asili yake ni nchini Korea kwa lugha
nyepesi unaweza ukauwita sanaa ya mapambano na pia unafanana na mchezo wa
karati lakini ni tofauti kabisa licha ya kuwa mchezo huo pia wanatumia kupiga mateke
na kurusha ngumi .
Mchezo huo unafundishwa katika ukumbi wa Judo Amani Mjini
Zanzibar na kocha Maxmiliana Kailangana kwa kila siku ya Jumatatu, Jumatano na
Alhamis kuanzia saa 1:00 usiku hadi 3:00 usiku huku kocha huyo akiwataka wadau
wengine kujitokeza kushiriki mchezo huo.
Comments
Post a Comment