SELEEMBE: TUTABEBA UBINGWA WA CHALENJ MWAKA HUU
Nahodha wa timu ya
Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Suleiman Kassim (Seleembe), amesema hakuna
wa kuwazuia kubeba Kombe la CECAFA SENIOR CHALLENGE CUP msimu huu kutokana na
ubora wa kikosi chao.
Seleembe ametamba
kuwa kasi waloanza kuonyesha haitosimama mpaka kubeba taji hilo kwenye
Mashindano ambayo yanaendelea nchini Kenya.
Nahodha huyo aliuambia
Mtandao huu kuwa, uwepo wa wachezaji vijana wanaotaka kufanikiwa itaongeza
chachu kupata matokeo, kitu ambacho walikikosa misimu uliopita.
“Tuna damu changa
ambayo inataka mafanikio, sasa itakuwa ngumu sana timu yoyote kutuzuia msimu
huu, tuna kila sababu ya kutwaa taji, vijana wanahamasa ya kupata mafanikio
katika maisha ya soka, hakuna wa kutuzuia katika hili,” alisema.
Zanzibar Heroes wanaongoza kundi A wakiwa na alama 6 baada
ya kuwafunga Rwanda 3-1 na jana kuwapiga kaka zao Tanzania bara 2-1 na kesho
Jumamosi watacheza mchezo wao wa tatu dhidi ya wenyeji Kenya, mchezo
utakaopigwa saa 10:00 za jioni katika uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos nchini
Kenya.
Endapo Heroes wakibeba kombe mwaka huu itakuwa ni kombe lao
la pili katika Mashindano hayo kufuatia kutwaa mara moja tu mwaka 1995, huku
mabingwa watetezi Uganda
ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa
wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na
Tanzania bara mara tatu.
Comments
Post a Comment