WACHEZAJI WA 4 WA ZANZIBAR HEROES WAPIMWA MKOJO, SASA WANASUBIRI MAJIBU KUTOKA AFRIKA YA KUSINI
Wachezaji wanne wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes)
leo saa 5 za usiku wamefanyiwa vipimo kama wanatumia dawa za kuongeza nguvu,vipimo
ambavyo vimefanywa na Mawakala wa kupinga utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu
Michezoni kupitia tawi lao nchini Kenya (World Anti-Doping Agency “WADA”) zoezi
ambalo limefanyika katika Hoteli ya Garden waliyokaa kambi timu hiyo iliyopo Machakos
Mjini Kenya.
Wachezaji waliyofanyiwa vipimo ni Kiungo Mohd Issa “Banka”,
Fesal Salum “Fei Toto” na Washambuliaji Ibrahim Hamad Hilika na Suleiman Kassim
“Seleembe”.
Hofu hiyo ilopelekea kupimwa wachezaji hao imekuja kwenye
Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup jioni ya leo katika uwanja wa Kenyatta
Mjini Machakos mara baada ya kutoka sare ya 0-0 na Wenyeji Kenya na kupelekea
Zanzibar kutinga moja kwa moja nusu fainali wakiwa na alama 7 wakiongoza kundi
lao A lenye Mataifa kama Kenya, Libya, Rwanda na Tanzania bara.
WADA na CECAFA wameingiwa na wasi wasi kutokana na kiwango
bora walichoonyesha Zanzibar katika Mashindano hayo huku ikiwaongoza mataifa
kama Libya, Rwanda, wenyeji Kenya na Tanzania Bara ambapo WADA na CECAFA waliwafata
wachezaji hao katika vyumba vya kubadilisha nguo baada ya kumaliza mchezo wa
leo lakini hawakufanikiwa kuwapima jambo ambalo limepelekea kuwafata mpaka
kambini kwao na kuwapima.
Awali walisema Wachezaji wa Zanzibar wana mashaka nao na
jinsi wanavyocheza si bure, hivyo baadae wakawataja wachezaji hao wanne akiwemo
kiungo kinda Fesal Salum “Fei Toto” ambae leo amechaguliwa kuwa nyota wa mchezo
wa leo kati ya Zanzibar na wenyeji Kenya ulomalizika 0-0.
Vipimo hivyo vitapelekwa Afrika ya Kusini kisha majibu
yatatoka badae.
“Tumeshawapima na hivi vipimo tunaenda navyo Afrika ya Kusini
kisha tutaleta majibu baada ya miezi 6”. Alisema mmoja wa Afisa kutoka World
Anti Doping.
Kwa upande wa Zanzibar Heroes wameshangazwa na jambo hilo
huku wakisema kuna mchezo mchafu unataka kufanywa na wenyeji wao.
“Sisi tuna wasi wasi na mchezo mchafu unataka kuchezwa hapa, Hoteli
yao, chakula chao, maji yao na kutupima wanatupima watu wao, sawa sisi
tumekubali kupimwa tunawasubiri na hayo majibu yao, mana hatuna wasi wasi
wowote sisi”. Alisema Kiongozi mmoja wa Zanzibar.
Tangu kuanza Mashindano ya Cecafa ya mwaka huu Zanzibar
inaongoza kutoa wachezaji bora wa mchezo yani Men of the Match ambapo mchezo wa
awali Zanzibar Heroes waliichapa Rwanda mabao 3-1 huku mchezaji bora akitajwa
kuwa Mohd Issa “Banka”, mchezo wa pili Zanzibar waliwafunga Tanzania bara mabao
2-1 na mchezaji bora wa mchezo akawa Ibrahim Hamad “Hilika” na leo Zanzibar 0-0
Kenya mchezaji bora pia katoka Zanzibar Fesal Salum.
Comments
Post a Comment