WAFUGAJI WA MANYARA HATA SOKA WAPO VIZURI

Timu ya jamii ya wafugaji wa Naisinyai S. C ya Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeshinda ngao ya maadili iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kuifunga Mirerani SC kwa penalti 6-5.

Katika mchezo huo wa fainali uliochezwa jana kwenye uwanja wa barafu mji mdogo wa Mirerani, mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Zuwena Omary.

Hadi dakika 90 ya mchezo ulipomalizika timu hizo zilikuwa hazijafungana na walipopigiana penalti tano kwa tano hakukuwa na mshindi ndipo wakapigiana penalti moja kwa moja na Naisinyai ikashinda.

Katibu Tawala huyo Zuwena akizungumza wakati wa kukabidhi ngao hiyo ya maadili kwa timu ya Naisinyai alisema jamii inapaswa kupiga vita matumizi ya vitendo vya rushwa kwa kila sehemu.

Alisema jamii inapaswa kuzingatia hilo kupitia kauli mbiu ya wajibika, piga vita rushwa, zingatia maadili, haki za binadamu na utawala bora kuelekea uchumi wa kati.

"Tupige vita rushwa kila mahali, kuanzia michezo ni, makazini, polisi, hospitalini, mahakamani na kila eneo ukiona rushwa inatumika toeni taarifa," alisema Zuwena.

Mkuu wa Takukuru wilaya ya Simanjiro Mashauri Elisante alisema mashindano hayo yalishirikisha timu nne za Naisinyai SC, Mirerani SC, Veterani Mirerani za Simanjiro na Tanzanite FC ya wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Elisante alisema lengo la mashindano hayo ni maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kitaifa na kupiga vita rushwa.

Alisema mshindi wa kwanza wa mashindano hayo amepata ngao na jozi moja ya sare za michezo, mshindi wa pili amepata mipira miwili na aliyeshika nafasi ya tatu na ya nne kila mmoja amepewa mpira mmoja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Taiko Laizer alisema hii ni mara ya pili kwa mwaka huu timu hiyo kubeba ubingwa wa soka kwani awali walishinda kombe la mbunge wa jimbo la Simanjiro James Ole Millya.

Laizer alisema siri ya ushindi mara mbili kwa mwaka mmoja kwenye timu hiyo ni kuzingatia mazoezi, nidhamu na ushirikiano wa uongozi na wananchi kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

WACHEZAJI WA 5 WA ZANZIBAR HEROES WAMEITWA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA TAIFA STARS KWAAJILI YA MICHEZO MIWILI YA KIMATAIFA YA KALENDA YA FIFA.

ZANZIBAR KARIBU WATAPATA UANACHAMA WA FIFA BAADA YA KUWA MWANACHAMA WA 55 WA CAF

JKU ACADEMY HAO WATANGULIA KWENDA ARUSHA KATIKA MASHINDANO YA ROLLING STONE