BALOZI SEIF AWEKA JIWE LA MSINGI UWANJA WA MAO TSI TUNG

Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ujenzi
wa Viwanja vya Michezo Nchini uliomo ndani ya Programu ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar unaudhihirishia Ulimwengu azma ya Zanzibar ya
kutaka kukuza sekta ya Michezo Nchini ili irejee katika hadhi yake
Kimataifa.

Amesema Viwanja hivyo vitakapokamilika vitaweza kusaidia uzalishaji wa Wanamichezo bora watakaoiweka Zanzibar katika Ramani ya Dunia
kimichezo kama walivyofanya Zanzibar Heroes na Wanakabumbu wa Soka la Ufukweni Zanzibar Beach Sand Heroes.

Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la
Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung ikiwa ni muendelezo wa harakati za shamra shamra za sherehe za maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Alieleza kwamba ujenzi wa Uwanja wa Mau Tse Tung ni jitihada kubwa
zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein katika kuendeleza michezo ambazo
zinastahiki kupongezwa na wanapenda michezo Nchini.

Balozi Seif alisema jitihada hizo tayari zimeanza kuonekana moja kwa
moja katika Mpango wa Ujenzi wa Viwanja vya Michezo katika Wilaya
zote Unguja na Pemba kwa kuanzia Kiwanja cha Kitogani ndani ya Wilaya ya Kusini katika Kisiwa cha Unguja.

Amesema Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung ambao unagharamiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni sehemu ya Mkakati wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015/2020 katika kuendeleza Sekta ya Michezo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Uwanja huo una historia kubwa kutokana na kupewa Jina la Rais wa mwanzo wa China Marehemu Mao Tse Tung jambo ambalo Wazanzibari wana kila sababu ya kujivunia kuwa miongoni mwa Nchi Tatu za Afrika ikitanguliwa na Senegal na Namibia zilizopata Heshima kutoka Taifa la China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Wanamichezo na Wananchi wote watakaopata fursa ya kuvitumia Viwanja hivyo baada ya kukamilika kwake kuendeleza Utamaduni wa kutunza mazingira yaliyo ndani ya Viwanja hivyo ili wafadhili wa Miradi hiyo waone kwamba misaada wanayotoa inaendelea kutunzwa na kuthaminiwa.

Aidha aliutaka Uongozi wa vyama vya Michezo kupitia Vilabu
wanavyovisimamia waanze kujipanga namna ya jinsi ya matumizi yake
hasa kwa kuzingatia Viwanja vyenyewe vinajengwa kwa ajili ya matumizi ya Jamii kwa ujumla wake.
Aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa
jitihada inazoendelea kuchukuwa katika kusaidia kugharamia ujenzi wa
Kiwanja cha Mao Tse Tung kikitanguliwa na kile cha mwanzazo cha Amaan kilichojengwa mnamo Miaka ya 70.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Zanzibar Omar Hassan King alisema Uwanja wa Mao Tse Tung utakaokuwa wa Kijamii zaidi tofauti na viwanja vyengine vya Michezo unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani Milioni Tano sawa na shilingi zaKitanzania Bilioni 15.

Alisema Bilioni 11 sawa ya Yuan Milioni 29 zinatolewa na Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China na Shilingi Bilioni 4 zitatolewa na
Sewrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuendeleza ujanei huo.
Omar Hassan alisema mradi wa ujenzi wa Uwanja huo unahusisha pia
uimarishwaji wa Miundombinu ikiwa ni pamoja na ujengaji wa viwanja
viwili vya Michezo wa Mpira wa Miguu ambavyo vyote vitawekewa Nyasi Bandia kwa lengo la kuwa na hadhi ya Kimataifa.

Alisema ipo sehemu itakayokuwa na Jengo la Michezo ya ndani { Indoor
Games } kwa ajili ya Mpira wa Meza, Wavu, Pete, Majengo Mawili kwa
matumizi ya Ofisi pamoja na kuwekwa zana na Vifaa vya mazoezi
vitakavyohimili hali zote za Hewa ukiwemo pia uzio utakaouzunguuka
Uwanja wote.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
aliishukuru Wizara ya Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi kwa kusaidia
Rasilmali ya Mchanga inayotumika zaidi kwenye ujenzi wa Mradi huo
ambao ndio changamoto kubwa iliyokuwa ikiwasumbuwa Wakandarasi wa Ujenzi huo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Pen Yang aliithibitishia Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwamba kazi ya ujenzi wa Uwanja wa Mao
itaendelea kutekelezwa ili ikamilike katika kipindi kilichopangwa.
Bwana Pen Yang Uwanja wa Michezo wa Mao utaendelea kubakia katika Historia ya Uhusiano wa muda mrefu ulkiopo kati ya China na Zanzibar ulioanza mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Mwakilishi huyoi wa Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alisema
kwamba Kiongozi wa Taifa la China alitia saini Mkataba wa ushirikiano
kati ya Nchi hiyo na Bara la Afrika ikihusishwa miradi tofauti ya
maendeleo ikiwemo Sekta muhimu ya Michezo.

Ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung uliopo Mtaa wa Mpirani
Kikwajuni ulioanza mapema Mwezi Mei Mwaka 2017 unafanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai Group ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapoMwezi Oktoba Mwaka huu wa 2018.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Omar Hassan Kingi akitoa maelezo ya kiutendaji wakati wa hafla
ya uwekaji wa jiwe la Msingi wa Uwanja wa Mao Tse Tung

Comments

Popular posts from this blog

HUYU NDIYE MCHEZAJI MWENYE REKODI YA KUFUNGA MAGOLI MENGI KWENYE MECHI YA TAIFA DHIDI YA BOYS