BALOZI SEIF USO KWA USO NA RAIS WA ZFF, WAPEWA USHAURI WA KUKUZA SOKA ZANZIBAR

Seif  Kombo Pandu kushoto na Kulia ya Balozi Seif

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushauri Uongozi Mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} kusimamia vyema Sheria pamoja na Kanuni ilizojiwekea za kuendesha Mpira wa Miguu ili kuepuka migogoro inayoweza kuviza viwango vya Soka Nchini.

Amesema wapo baadhi ya Viongozi waliowahi kushika madaraka ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar lakini walishindwa kuzitekeleza sheria hizo na hatimae walifikia hatua ya kupelekana Mahakamani jambo ambalo linakwenda kinyume na uendeshaji wa Vyama vinavyosimamia na kuendesha soka Kitaifa na Kimataifa.

Akizungumza na Uongozi Mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} hapo Afisini kwake Vuga, Balozi Seif Ali Iddi amesema vurugu zilizokuwa zikishuhudiwa kutokea ndani ya Uongozi wa iliyokuwa ZFA kipindi cha nyuma zilichangia kudorora kwa kiwango cha Soka hapa Nchini.

Balozi Seif amesema Uongozi huo wa sasa unapaswa kuelewa kwamba wao ndio watakaobeba lawama zitakazotolewa na Wapenzi wa Soka Nchini endapo kiwango cha Soka kitaonekana kushuka miongoni mwa Wachezaji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi huo Mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} kwa kuchukuwa madaraka katika kipindi cha mpito akiwa na matumaini makubwa ya kuimarika kwa mchezo wa Soka katika kipindi kifupi kijacho Nchini.

Amesema katika kuimarisha Sekta ya Michezo Nchini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaamua kujikita katika ujenzi wa Viwanja vya Michezo katika kila Wilaya Unguja na Pemba ikiwa ni muendelezo wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi huo Mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar kwamba Serikali itakuwa tayari kutoa kila msaada utaohitajika katika kuona Sekta ya Michezo hasa Mchezo wa Soka unaopendwa zaidi inaendelea kuimarika kila siku.

Mapema Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} Seif  Kombo Pandu alisema  Shirikisho hilo limejipanga kuendesha Soka kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Shirikisho la Soka Duniani {FIFA},Shirikisho la Soka la Afrika {CAF}na lile la Afrika Mashariki { CECAFA }.

Seif alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mipango hiyo ni pamoja na kujiwekeza zaidi katika miradi itakayolipatia mapato ya uhakika Shirikisho hilo ili lijiendeshe katika misingi inayokubalika.

Amesema ni vyema kwa Serikali kupitia Wizara inayosimamia Sekta ya Michezo kuridhia Mashindano ya Kombe la Mapinduzi {Mapinduzi Cup}ambayo ndio mashindano makubwa Tanzania yasimamiwe na Shirikisho hilo.

Ameeleza kwamba hatua hiyo itasaidia sana kuondoa nadharia ya shughuli za Michezo katika kuendesha Mashindasno hayo kusimamiwa na Kamati zilizo nje ya Taasisi zinazosimamia Sekta hiyo.

Rais huyo wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} ametoa wazo katika kuyapa nguvu zaidi Mashindano ya Kombe la Mapinduzi umefika wakati wa kuandaliwa Timu ya Kombaini inayotokana na Wachezaji wazuri wanaoshiriki Mashindano ya Ligi za Mitaani za Ndondo Cup kuingizwa katika Mashindano hayo makubwa.

Seif amesema Ligi za Ndondo Cup hapa Nchini zimekuwa na mashabiki wengi na kuchukuwa mvuto mkubwa unaopelekea Mji kurindima wakati wa hatua za Nusu Fainali na Fainali kamili ya Mashindano hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Uongozi Mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar {ZFF} uliofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisharasmi.


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

HUYU NDIYE MCHEZAJI MWENYE REKODI YA KUFUNGA MAGOLI MENGI KWENYE MECHI YA TAIFA DHIDI YA BOYS